Ajali ya MV Spice Islander
General Description
Source: Zenjishoppazz
Release date: 2023-02-23
TUKIO LA KUZAMA KWA MELI YA MV SPICE ISLANDER
Mnamo siku ya tarehe 10 Septemba 2011, watu wa visiwa vya Unguja na Pemba, na Tanzania kwa ujumla waliamka huku wakiwa na majonzi, na simanzi za hali ya juu baada ya kuzagaa mithili ya umeme taarifa za kuzama kwa meli ya MV Spice Islander katika mkondo wa Nungwi Visiwani Zanzibar. Meli hiyo ilikuwa ikitokea katika kisiwa cha Unguja na kuelekea Pemba.
Kwa hakika siku hiyo ilikuwa ni siku iliyojaa majonzi, huzuni na vilio kwa taifa la jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kukutwa na msiba mzito ambao ulitonesha vidonda na majeraha ya watu wengi, na kupelekea kuikumbuka ajali nyengine kubwa iliyolikumba taifa la Tanzania, nayo ni Ajali ya MV Bukoba iliyotokea mnamo tarehe 21 Mei 1996. Ajali hiyo ambayo ilitokea wakati meli ilipokua inakaribia bandari ya Mwanza kwa umbali wa kilometa 56, ilizama katika ziwa Victoria katika kimo cha maji chenye urefu wa mita 25, na kusababisha vifo vya Zaidi ya watu 894.
Kwa mujibu wa taarifa ya ripioti ya Tume iliyochunguza Kuzama kwa Meli hiyo ya MV Spice Islander iliyotolewa mwezi wa Februari, mwaka wa 2012, idadi ya maiti zilizopatikana na kuzikwa ni 243, huku watu 941 wakiokolewa wakiwa hai.
Idadi kubwa zaidi hata hivyo, inaaminika ni ya wale waliokuwa hawakupatikana. Mali nyingi pia zilipotea na hadi sasa bado haijawahi kujuilikana hasa thamani kamili ya mali hizo wala idadi kamili ya wahanga wa Spice Islander, ingawa watu waliotajwa kufa na kupotea hadi kutolewa kwa ripoti hiyo ni 1370.
Msiba huu unatajwa kuwa mkubwa kabisa katika historia iliyoko kwenye rikodi ya visiwa vya Unguja na Pemba, kwa watu wengi kufariki kwa pamoja katika mkasa mmoja baharini.
Katika mapendekezo yake, tume hiyo iliyoundwa kuchunguza tukio la kuzama kwa meli ya MV Spice, ilitaka hatua kadhaa za kisheria na kinidhamu kuchukuliwa kwa baadhi ya waliohusika, kwa namna moja au nyengine aliyepelelekea kuzama kwa meli hiyo. Na pia kwa kupatiwa msaada, kwa wale wote waliopoteza ndugu, jamaa na mali zao kupitia ajali ya Spice Islander.
Mwaka mmoja baadaye, waziri wa miundombinu na mawasiliano wa Zanzibar, Rashid Seif, alisema kuwa serikali imejipanga kukabiliana na majanga makubwa ya baharini, na kwamba majanga kama hayo hayatotokea tena, ingawa hata miezi miwili haijatimia tangu kuzama kwa meli ya Spice Islander, ilizama meli nyengine ya Mv Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Unguja.
Kwa hakika, hakuna jicho lenye huruma lililojizuia kutokwa na machozi kutokana na msiba huu mzito na mkubwa kwa Tanzania. Pia Karibu dunia nzima iliungana Pamoja na Watanzania katika kipindi hiki kigumu cha simanzi na majonzi ya hali ya juu kabisa.
MV Spice Islander Ilijengwa mwaka 1967 na ikijuilikana kama Marianna kwa mmiliki asiyejulikana, baadaye aliuzwa kwa Theologos P. Naftiliaki wa Ugiriki. Mnamo mwaka 1988, Marianna iliuzwa kwa Apostolos Shipping na kuitwa Apostolos P. Baadaye iliuzwa kwa kampuni ya Saronikos Feri.
Mnamo mwaka 2005, Apostolos P alisajiliwa na kampuni ya Hellenic Seaways. Na ilipofika Mwaka 2007, aliuzwa kwa Makame Hasnuu wa Zanzibar, Tanzania, na kuitwa Spice Islander I.
Tarehe 25 Septemba 2007, Spice Islander I ilipokuwa nje ya pwani ya Somalia ikielekea zake Tanzania ilipata matatizo katika injini yake kutokana na mchanganyiko wa mafuta machafu. USS Stout kutoka Combined Task Force 150 ilitumwa kuisaidia meli hiyo iliyopata matatizo baharini.
Meli hiyo ya MV Spice Islander ilikuwa safarini ikitokea Oman kuelekea nchini Tanzania, na haikuwa na abiria yoyote yule ndani yake. USS James E. Williams pia ilijibu kwa kuitika muitiko huwo wa tahadhari uliotolewa na MV Spice Islander. Stout aliipatia meli hiyo galoni 7,800 (lita 30,000) za mafuta na kuwapa wafanyakazi kumi wa kuwasaidia, chakula pamoja na maji. Baada ya injini zake kuwashwa upya, alianza tena safari yake ya kuelekea Zanzibar -Tanzania.
Hapana shaka, Mola amekwisha kadiria na kuchukua amana zake, na kwake ndiko kwenye marejeo ya viumbe vyote. Lakini pia, kama alivyosema Sabri Juma ambae ni muhanga wa ajali ya MV spice wakati alipohojiwa na Shirika la habari la Ujarumani (DW), na kama ilivyogundulika na tume ya uchunguzi wa ajali hiyo, ya kwamba ajali hiyo ilsababishwa na uzembe uliotokana na orodha ndefu ya wahusika ambao kwa hali moja au nyengine walichangia kutokezea kwa ajali hiyo, huwezi kuekwa kando orodha hiyo kwenye maafa haya makubwa yaliyoikumba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla mnamo mwaka wa 2011.
Others
- Ifahamu Museum for the Future Dubai
- The Motivation Myth
- TABIA 12 ZA MATAJIRI/MAMILIONEA
- Mambo saba ya kujifunza katika kitabu cha The Richest Man in the Babylon
- History Form One Notes
- KARIBU USAFIRI NASI KWA SAFARI YA HIJA
- MAMBO SABA WANAYOYAFANYA MASKINI, AMBAYO MATAJIRI HAWAYAFANYI
- NAMNA NZURI YA KUWEZA KUHIFADHI PESA